Zelensky akaribia kukubali kupatia Trump madini ya Ukraine kwa usaidizi wa vita – Taifa Leo


WASHINGTON D.C, AMERIKA

SIKU chache baada ya Rais wa Amerika, Donald Trump kumwita mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy dikteta, viongozi hao wanakaribia kukubaliana kuhusu mkataba wa madini.

Mkataba huo utahakikisha kuwa Amerika inanufaika kwa utajiri wa madini ya Ukraine na kurejeshewa pesa na msaada wa kijeshi ambao imeipa Ukraine kwenye vita dhidi ya Urusi.

Ukraine ambayo imekuwa na uhasama mkubwa baina yake na Rais Trump, inaelekea kukubali mkataba huo ili Amerika iisaidie kumaliza vita dhidi ya Urusi.

Na iwapo vita hivyo vitaendelea, Ukraine itatarajia msaada zaidi kutoka kwa Amerika ili kujilinda.

Rais Trump aliahidi kumaliza uhasama wa kivita kati ya Ukraine na Urusi na pia ameshiriki mazungumzo na Rais Vladimir Putin, kusaka suluhu kwa vita ambavyo vimedumu kwa muda wa miaka mitatu.

“Kile tunafanya hapa ni kuhakikisha kuna usalama na amani. Walipa ushuru wa Amerika nao watapata pesa zao ambazo zilitumika Ukraine,” akasema Rais Trump.

Mtangulizi wa Rais Trump, Rais Mstaafu Joe Biden, wakati wa utawala wake, alikuwa ametoa msaada wa kifedha na kijeshi kwa Ukraine ili ijilinde dhidi ya kuvamiwa na Urusi.

Zelenskiy alikataa kutia saini pendekezo la awali kwa kuwa Rais Trump alikuwa anataka nchi yake inufaike kwa utajiri wa madini ya Ukraine ya thamani ya Sh64 bilioni.

Ukraine ilisema ilipokea msaada ambao haufiki kiwango hicho na mkataba huo haukuwa na hakikisho la masuala yote waliyoyahitaji.

Trump alisema huenda Zelenskiy akafika Ikulu ya White House, Amerika Ijumaa kesho ili watie saini mkataba huo wa madini na kukubalia mchakato wa kumaliza vita dhidi ya Urusi.

Alipomrejelea Zelenskiy kama dikteta, Rais Trump pia alidai kuwa rais huyo ndiye alianzisha vita dhidi ya Urusi, madai ambayo yalikashifiwa na raia wa Ukraine.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*